 |
UTARATIBU WA UTOAJI WA PASIPOTI MPYA |
Serikali ya Tanzania iliamua kutoa pasipoti mpya zinazosomeka kwa mashine(Machine readable passports), ambazo zilianza kutumika rasmi tarehe24/3/2005. Pamoja na mambo mengine, zoezi la kutoa pasipoti hizo linalenga katika kudhibiti pasipoti zetu. Serikali imetoa muda wa miezi sita (yaani hadi Septemba 23, 2005) kwa pasipoti zote za zamani kubadilishwa. Baada ya hapo pasipoti hizo hazitatambuliwa tena.
Ili kukidhi madhumuni ya kutoa pasipoti mpya, utaratibu ufuatao utatumika kwa wote watakaooomba pasipoti hizo kupitia Balozi zetu:-
- Uandikaji wa pasipoti zote utafanywa na Makao Makuu ya Uhamiaji pamoja na Zanzibar.
- Balozi zitashughulikia na kuidhinisha maombi yote ya pasipoti hizo mpya kwa raia wa Tanzania waishio nje ya nchi na kisha kuyatuma Makao Makuu kwa Mkurugenzi wa Uhamiaji. Baada ya uhamiaji kuandika pasipoti, itazituma Ubalozini ili ziwasilishwe kwa wahusika.
- Ada ya pasipoti:-
Fomu za maombi ya pasipoti zitalipiwa US$ 10 kila moja na pasipoti italipiwa US$ 40. Hivyo malipo yote ni US$ 50. Izingatiwe kwamba, iwapo mwombaji wa pasipoti atajaza vibaya, ataharibu au kuchafua fomu ya maombi, atalazimika kununua/kulipia fomu nyingine kwa US$ 10.
- Fomu za maombi:-
Fomu za maombi zinapatikana Ubalozini. Mwombaji anashauriwa kutembelea tovuti ya Ubalozi ili kusoma maelezo ya fomu hiyo na kuandaa taarifa zote muhimu na vitu vinavyotakiwa kuwasilishwa wakati wa kuomba pasipoti mpya. Fomu halisi itajazwa wakati atakapoonana na Afisa wa Pasipoti.
- Mwombaji wa pasipoti akishajaza fomu ya maombi, ataweka sahihi yeye mwenyewe mbele ya afisa wa pasipoti/Ubalozi kwa kutumia kalamu maalumu. Aidha mwombaji huyo atachukuliwa alama za vidole na afisa wa pasipoti/Ubalozi.
- Picha:-
Mwombaji wa pasipoti anatakiwa kuwasilisha nakala tano(5) za picha ya pasipoti zenye rangi ya bluu bahari kwa nyuma(a light blue background). Picha hiyo iwe yenye urefu wa 4.5 sentimeta na upana wa 4.0 sentimeta(4.5×4.0 cm).
- Mwombaji atatakiwa kuambatanisha maombi yake na pasipoti aliyokuwa nayo kwa ajili ya kuithibitisha, pamoja na nakala za ukurasa wa 1 - 4, ukurasa wa mwisho wenye namba ya faili, ukurasa wenye visa au kibali cha kuishi mahali alipo (resident permit) pamoja na nakala ya “Certificate of Alien Registration" kwa wale waishio Japan.
- Hati nyingine zinazotakiwa kuambatanishwa na maombi ya pasipoti ni kama ilivyoorodheshwa katika fomu za maombi. Mwombaji anapaswa kuwasilisha hati hizo ikiwa hakuwa ameziwasilisha katika maombi ya pasipoti ya zamani.
- Mwombaji ataruhusiwa kubaki na pasipoti yake mpaka hapo pasipoti mpya itakapotumwa Ubalozini. Akishaarifiwa kuwasili kwa pasipoti yake, mwombaji ataituma pasipoti ya zamani kwa "Registered mail", ili iweze kufutwa na kisha kurudishwa kwake ikiambatanishwa na pasipoti mpya.
|